Friday, March 2, 2018

Wanaokaa Mabondeni Waonywa na TMA, Mamlaka ya Hali ya Hewa Yatabiri Mvua Kubwa


WAKATI mvua kubwa zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kunyesha mwezi huu zikianza jana jijini Dar es Salaam, TMA kwa mara nyingine imewaonya wakazi wa mabondeni kuwa ni kubwa na zinaweza kusababisha mafuriko.

TMA ilisema mvua zilizoanza jana zinatarajiwa kuongezeka katika baadhi ya maeneo ya kati ya nchi kuanzia leo, hivyo ni vyema wakazi wa mabondeni wakachukua tahadhari ikiwamo kuhama maeneo hatarishi.

Taarifa iliyotolewa na TMA katika mtandao wake wa kompyuta jana ilisema kutakuwa na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo machache ya ukanda wa Ziwa Victoria.

Ilitaja sehemu nyingine kuwa maeneo ya magharibi na katikati mwa nchi, nyanda za juu kaskazini mashariki, nyanda za juu kusini magharibi na mkoa wa Morogoro.

"Tahadhari, onyo, kuna angalizo la matarajio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo nchini," ilieleza tarifa hiyo.

Aidha, TMA ilitaja mikoa itakayoathirika na mvua, vipindi vya jua pamoja na hali ya mawingu kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe, Iringa, Songwe, Kagera na Geita.

Mingine ni Mara, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Shinyanga, Simiyu, Dodoma na Singida, Ruvuma, Morogoro, Lindi na Mtwara, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba.

Februari 15 TMA ilitahadharisha wananchi kuwa mvua kubwa za vipindi vifupi za masika zinatarajiwa kunyesha mwezi huu hadi Mei, na zinaweza kusababisha mafuriko na athari katika sekta mbalimbali.

TMA ilieleza kuwa katika kipindi hicho mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi nchini.

Pia ilisema kutakuwa na ongezeko la maji katika mabwawa, kwenye maeneo ambayo yatakuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger