Sunday, March 4, 2018

Wananchi wa Dar Es Salaam Kuunganishiwa Gesi Asilia Kwa Matumizi ya Majumbani


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) kuharakisha uunganishaji wa huduma ya gesi asilia katika baadhi ya nyumba za wananchi kwenye maeneo ya jiji la Dar Es Salaam kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Dkt.Kalemani aliyasema hayo ofisini kwake mkoani Dodoma alipokutana na watendaji wa TPDC kwa lengo la kujadili suala la usambazaji wa Gesi asilia katika nyumba za Wananchi pamoja na bei watakayouziwa wananchi hao.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kalemani aliwataka TPDC kuunganisha nyumba kuanzia Hamsini( 50) na kuendelea, na huduma ya gesi asilia katika maeneo la Mwenge na Mikocheni, kwa kuwa tayari miundombinu ya bomba la gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani imepita maeneo hayo.Wakizungumzia suala la bei ya kuwauzia wateja, Dkt. Kalemani alisema kuwa pamoja na mambo mengine Gesi hiyo itauzwa kwa Wananchi kwa pungufu ya 40% ya bei ya mitungi ya gesi itayokuwa sokoni kwa wakati huo.

" Hii ni gesi yetu na bomba ni la kwetu vyote vinapatikana hapahapa nchini, ni vyema iuzwe kwa bei ya chini zaidi ya ile iliyopo sokoni kwa sasa, ili kila mwananchi aweze kumudu gharama zake pia ni rafiki wa mazingira, itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kulinda misitu yetu", alisema Dkt. Kalemani. 
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger