Thursday, March 1, 2018

Wakili Ataka Ndama ‘Mtoto wa Ng’ombe’ Afutiwe KesiUpande wa utetezi katika kesi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mfanyabiashara , Ndama Hussein maarufu Pedeshee Ndama mtoto ya Ng’ombe, umeuomba upande wa mashtaka kuifuta kesi hiyo hadi pale upelelezi wa shtaka hilo utakapokamilika.

Ndama anakabiliwa na mashtaka matano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yanayohusiana na kughushi na kujipatia kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Dola 540,000 za Marekani.

Wakili wa utetezi, Jeremia Ntobesya amedai hayo leo Jumatano Februari 28, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa kudai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Msigwa amedai kuwa licha ya upelelezi kutokamilika, pia wameongea na maofisa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili waweze kuandika barua ya kukumbusha kuhusiana na nyaraka wanazosubiri kutoka nchini Australia.

“Mheshimiwa, sehemu ya upelelezi iliyobaki ni ile iliyopo nje ya nchi na kwa kutambua haki za mshtakiwa, ndio maana tumeanza kwa kuwaandikia barua ya kukumbusha wenzetu kuhusiana na nyaraka tunazosubiri kutoka nchini Australia na ikishindikana tutafanya maamuzi mengine ” amedai wakili Msigwa

Baada ya maelezo ya Msigwa, wakili wa Ndama, Mtobesya amedai kuwa mteja wao ana haki ya kuwa huru, “Hivyo naomba upande wa mashtaka kama mnaona bado hamjakamilisha upelelezi wenu, muifute kesi hii hadi pale mtakapokamilisha  upelelezi wenu, ili mteja wangu aweze kuwa huru kuendelea na shughuli zake.”

“Mtakapokamilisha  upelelezi wenu na kujiridhisha, ndio mumkamate na kumfungulia kesi tena.”

Kutokana na hoja za pande zote, Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo hadi March 27, 2018 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Hata hivyo, hii ni mara ya tatu kwa kesi hiyo kuahirishwa tangu upande wa mashtaka walipodai mahakamani hapo kuwa wanasubiri nyaraka kutoka Australia.

Katika kesi ya msingi, Ndama anadaiwa kuwa  Februari 20, 2014 Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la pili,  anadaiwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la tatu, Ndama anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionyesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.

Pia anadaiwa kuwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd akionyesha kampuni ya Muru imeyawekea bima maboksi manne yaliyokuwa na dhahabu hizo.

Katika shtaka la tano, anadaiwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade TJL DTYL Limited Dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya atawapa na kusafirisha dhahabu hizo.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger