Monday, March 5, 2018

Wadau Washauri Mambo Matano Kuunda Katiba Mpya


Dar es Salaam. Wakati vuguvugu la mchakato wa kuunda Katiba mpya likiibuliwa upya na Serikali ikishinikizwa kuufufua, wadau wameshauri mambo matano yafanyiwe kazi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 na ule wa Serikali za mitaa mwakani.

Hata hivyo, Serikali ilieleza msimamo wake kuwa kwanza ni kushughulikia huduma za kijamii, Hivi karibuni, kumekuwapo na kauli kutoka kwa wanasiasa, wanaharakati, wananchi na viongozi wa dini wakisema ili kuwepo na utawala bora na chaguzi huru na za haki ni lazima iwepo Katiba mpya, Makundi hayo yamedai kuwa Katiba iliyopo sasa ya mwaka 1977 imepitwa na wakati.

Kauli, mijadala na makongamano yaliyofanyikia chini ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), asasi za kiraia, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) yameonyesha hofu inayoweza kujitokeza katika chaguzi zijazo kama mfumo unaotumika sasa utaendelea pasipo na mabadiliko yoyote.

Jana, Mwananchi lilizungumza kwa nyakati tofauti na wadau mbalimbali kuhusu mkwamo wa mchakato wa Katiba mpya na njia zinazoweza kutumika ili chaguzi zijazo ziwe huru na za amani, Wadau hao walieleza mambo matano wanayoona yanahitaji kufanyiwa mabadiliko ya kisheria.

Mambo hayo ni Tume huru ya uchaguzi, Sheria ya Jeshi la Polisi na jeshi hilo liwe linatoa huduma, usalama wa Taifa uwe nje ya mfumo wa siasa, mgombea binafsi na matokeo ya Rais yahojiwe mahakamani.

Katikati ya mijadala ya mapendekezo hayo, swali linabaki je Serikali iko tayari kusikia na kuifanyia kazi mitazamo ya wadau hao? Je muda uliobaki kufika mwakani unatosha na iwapo fedha za kuendeleza mchakato zipo?

Alipotafutwa na Mwananchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi alisema mabadiliko ya muundo na haki za binadamu yanasimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria hivyo akaeleza atafutwe waziri ambaye ni Profesa Palamagamba Kabudi.

Hata hivyo, Profesa Kabudi hakupatikana kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokewa huku msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akisema; “Msimamo wa Serikali ni ule ule, ukifika wakati tutakamilisha kiporo.”

Kuhusu mapendekezo ya kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ili kuwepo na Tume huru ya uchaguzi, Dk Abbasi alisema, “yote hayo ya Tume huru na mengine wakati ukifika utakamilishwa na wala hakuna haja ya shinikizo.”

Dk Abbasi anatofautiana na kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema alipendekeza mambo matatu yafanyike kabla ya chaguzi zijazo kuwa ni; “kubadilishwa sheria ya uchaguzi na kuweka Tume huru ya uchaguzi, ibadilishwe sheria ya Polisi na kulifumua jeshi ikiwamo kuliondoa kutumika kisiasa.”

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini aliongeza kuwa sheria ya usalama wa Taifa ibadilishwe na kitengo hicho kiwe nje ya mfumo wa siasa.

Alisema endapo mapendekezo hayo hayatafanyiwa kazi chaguzi zijazo, “zitakuwa mbaya kuliko uchaguzi mdogo wa Kinondoni.”

Mratibu wa Mtandao wa Wapiganiaji wa Haki za Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa alisema Katiba hata ikipatikana huchukua muda kuanza kutumika kwani lazima kufanyike mabadiliko ya sheria na vitu vingine, hivyo ili chaguzi zijazo zifanyike vyema mabadiliko ya sheria hayana budi kufanyika. “Hili la mgombea binafsi tena ni mahakama ya kimataifa ilitoa hukumu, matokeo ya Rais yahojiwe mahakamani kama Kenya wanavyofanya, Tume huru ya uchaguzi na watendaji wake wapatikane kwa uwazi na iwe na watumishi nchi nzima,” alisema Ole Ngurumwa.

“Kwa hali tuliyonayo sasa, hadi Katiba ipitishwe na kuanza kufanya kazi itachelewa kwa hiyo tufanye mabadiliko ya sheria na hili la mawaziri wasiwe wabunge ni la muhimu ili kuondoa mgongano wa kimaslahi kama lilivyopendekezwa katika rasimu ya Jaji Warioba.”

TLS yazungumzia utekaji
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Godwin Ngwilimi alisema uchaguzi si Katiba pekee, kwani hata Katiba au sheria zilizopo haziruhusu. “Mtu kuteka watu, msimamizi wa uchaguzi kukataa kuwatendea haki mawakala wa chama fulani hili si suala la Katiba,” alisema.

“Tunataka Tume huru. Ili tuwe na uchaguzi huru na haki ni lazima tutengeneze vigezo na vigezo hivyo tukubaliane navyo, watu wa aina gani wanateuliwa, mamlaka ya Tume ni yapi, uwezo na nguvu ya Tume yenyewe itakuwa ni ipi.”

“Ni lazima kuwepo mjadala wa kitaifa ukijumuisha viongozi wa siasa, dini, wananchi, wataalamu wa masuala ya sheria na Katiba na hata ikiwezekana wataalamu wa nje ya nchi waitwe kama walivyofanya Kenya na mkifikia mwafaka mnabadili sasa sheria.”

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Katiba si uchaguzi kwa kuwa hata Katiba na sheria zilizopo licha ya upungufu wake bado hazifuatwi na viongozi waliopo madarakani wanafanya wanavyotaka.

Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger