Monday, March 5, 2018

Simba: Yanga Hawapaswi Kuchekelea Wao Ndiyo Watatupa Ubingwa


SARE ya Simba dhidi ya Stand United ni kama imewaamsha Yanga kutetea ubingwa wao lakini uongozi wa timu hiyo, umeweka wazi kuwa Yanga hawapaswi kuchekelea matokeo hayo kwani ubingwa wa msimu huu wataupata kutokea kwao.

Simba ilitoka sare ya bao 3-3 na Stand katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa huku matokeo hayo yakiibakiza kileleni ikiwa na pointi 46 baada kucheza michezo 20 huku Yanga wakiwa nafasi ya pili na pointi 40 na ikiwa na mchezo mmoja mkononi kufuatia kucheza mechi 19.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa matokeo waliyopata katika mchezo dhidi ya Stand ni kama yamewatoa usingizini kwani wameshapanga mkakati mzito utakaoweza kuwapa ubingwa wa msimu huu.

“Kiukweli matokeo ya sare dhidi ya Stand kwanza hatukuyategemea kabisa lakini imetokea, mashabiki hawapaswi kulalamika na watambue haiwezekani kila siku tushinde sisi, ila kitu kizuri ni kwamba hatujafungwa, sasa hao wanaoshangilia sijui wanashangilia kitu gani.

“Stand wametuamsha sasa tunaelewa na tumeweka mkakaki mzito wa kuhakikisha tunachukua ubingwa wa msimu huu na hatutaki yajirudie ya msimu uliopita lakini hao wanaoshangilia sare yetu wakumbuke tuna mechi nao ambayo tutawafunga na kuweza kuchukua ubingwa wa msimu huu,” alisema Manara.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Aprili 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa ligi kuu.


Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger