Monday, March 5, 2018

Kamati ya Kuchunguza Mauaji ya Faru Kileo YaundwaDar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema wameunda kamati kuchunguza mauaji ya faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti aliyemtaja kwa jina la Faru Kileo.

Faru Kileo aliuawa Desemba mwaka jana katika hifadhi hiyo na hadi sasa hakuna taarifa kamili iliyotolewa huku watendaji waandamizi wa wizara hiyo waliozungumza na Mwananchi siku tatu zilizopita wakitoa kauli zinazokinzana.

Wakati katibu mkuu wa wizara, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akisema unafanyika uchunguzi wa kawaida, Naibu Waziri Japhet Hasunga alikaririwa alisema unafanyika uchunguzi wa kina ukihusisha kuundwa kwa kamati maalumu.

Licha ya kusema kuna uchunguzi wa kawaida, Meja Jenerali Milanzi alikanusha pia madai ya kuhojiwa viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa).

Meneja mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa wanawashikilia watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuwa miongoni mwa mtandao wa ujangili na mauaji ya faru katika hifadhi hiyo.

Lakini, jana Dk Kigwangalla alipoulizwa kuhusu faru huyo alisema, “Kuna faru aliyejulikana kwa jina la Kileo aliuawa na majangili. Baada ya kuletewa taarifa za kifo chake tuliagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili tujue alivyouawa, tuwajue waliomuua na hatimaye tutathmini hali ya usalama wa faru wetu waliopo eneo hilo ambalo lipo mpakani na nchi jirani ya Kenya.”

“Mradi huu wa faru upo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na faru ameuawa jirani na vigingi vya mpaka wa kimataifa. Tumeunda kamati kuchunguza mauaji haya ya Faru Kileo na tutatoa taarifa rasmi uchunguzi utakapokamilika, japokuwa mradi huu unaendeshwa vizuri na kwa mafanikio makubwa lakini ni lazima tujiridhishe kama tuko salama kiasi gani.”

Ufafanuzi wa wizara
Katika ufafanuzi wake, Meja Milanzi alisema mauaji ya faru ni ya kawaida na kwamba kuna uchunguzi wa kawaida unaendelea kuhusu hilo.

“Ni kweli. Mara nyingi huwa ni ‘routine investigation’ inafanyika lakini si kuwahoji viongozi wa Tanapa. Ikitokea ‘incident’ (tukio) yoyote kama mnyama amekufa au ameuawa kunakuwa na ‘routine investigation’. Huwa ni kwenda field (eneo) pale wanapotupa taarifa. It’s a normal investigation (ni uchunguzi wa kawaida),” alisema.

Alisema Tanapa waliwapa taarifa mapema na walishaanza kufuatilia na kwamba licha ya mauaji ya mnyama huyo, bado faru wapo wengi japokuwa hakutaja idadi.

Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger