Friday, February 2, 2018

Hizi Hapa Hatari za Kunenepa Kupita Kiasi

Kunenepa kupita kiasi kunaweza kusababisha matatizo makubwa ya afya. Dakt. Scott Loren-Selco, mtaalamu wa mfumo wa neva katika Kituo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Southern California, anaonya kwamba hata vijana walionenepa kupita kiasi wanakabili hatari ya kupata Aina ya 2 ya ugonjwa wa kisukari. (Ona Amkeni! la Mei 8, 2003.) Anasema hivi: “Tunaona wengi wakiugua ugonjwa huo siku hizi, na inaogopesha sana. Mimi huwaambia [watu walionenepa kupita kiasi] kwamba ninaweza kuwapeleka kwenye chumba cha wagonjwa wa kisukari ili niwaonyeshe madhara wanayoweza kupata: hiyo inatia ndani vipofu, watu waliokatwa miguu, na watu wengi sana ambao wamelemazwa kabisa na aina ya 2 [ya kisukari]—kwa sababu ya kunenepa kupita kiasi.” Ni nini husababisha hali hiyo? Loren-Selco anasema hivi: “Kwa sababu wana pesa, wao hununua mikate mikubwa iliyotiwa nyama katikati na chipsi. Hakuna anayewaonya kwamba kula vyakula vingi vya aina hiyo kutawafanya wanenepe kupita kiasi, iwe ni wenye biashara hizo za chakula, au madaktari ambao hawajafundishwa kuhusu lishe.”

Dakt. Edward Taub, mwandishi maarufu kuhusu lishe, anasema: “Hivi karibuni, watu wameamini kwamba kunenepa sana ni jambo la kawaida na linalokubalika maishani. Wazo hilo la ajabu linaendelezwa na wenye biashara za chakula ambao hupata faida kwa kutunenepesha.”

Wataalamu wanasema kwamba watu walio na mafuta mengi mapajani huenda wakawa na afya nzuri kuliko wale walio na mafuta mengi tumboni (hasa ikiwa kiuno chao kinazidi sentimeta 90 hadi 100). Kwa nini? Kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight kinasema kwamba “kuwa na mafuta tumboni huongeza uwezekano wa kupanda kwa shinikizo la damu, kupata ugonjwa wa moyo, kisukari, kiharusi, na aina fulani za kansa. Ikiwa una nyonga kubwa, mapaja manene, na matako makubwa, basi hukabili hatari kubwa sana ya afya.”

Hivyo, mamilioni ya watu wazima na watoto ulimwenguni pote ambao wamenenepa kupita kiasi na wanakabili uwezekano wa kupata magonjwa hatari wanaweza kufanya nini? Je, kuna matibabu yanayofaa?
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger