Wednesday, December 20, 2017

Wasira Afunguka Kuongoza Mara Mbili Kupata Kura NEC-CCM

Mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira ametoa siri ya kuongoza kupata kura nyingi katika vipindi viwili tofauti katika uchaguzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi.

Katika uchaguzi wa NEC wa mwaka 2012, Wasira alipata kura zaidi ya 2,100 na kuwaongoza wenzake wote jambo ambalo limejirudia juzi.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Wasira ambaye juzi aliongoza kwa kupata kura 1,505 na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa NEC alisema hiyo inaonyesha jinsi wanachama wenzake wanavyomkubali ndani ya chama hicho.

Alisema anaamini mambo mengi yamechangia kukubalika kwake ndani ya chama hicho ikiwa ni pamoja na jinsi alivyotetea msimamo wa CCM wakati wa mchakato wa Katiba mpya.

“Wakati wa mchakato wa Katiba mpya, msimamo wa CCM ulikuwa ni Serikali mbili, tuliamini kuwa ili kuwe na muungano imara ni lazima kuwe na Serikali mbili, na hata mimi msimamo wangu ulikuwa hivyo,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Bunda.

Alisema kulikuwa na mijadala mingi ambayo iliendeshwa maeneo mbalimbali huku CCM ikitetea msimamo wake na vyama vya upinzani vikiwa na msimamo tofauti.

“Wakati huo nilikwenda kwenye mdahalo wa wazi pale Blue Pearl (Ubungo Plaza). Ilikuwa ni mdahalo wa Katiba kuanzia saa tisa alasiri mpaka 12:00 jioni, nilizungumza msimamo wa chama changu na kutoa hoja za msingi, niliwashinda Profesa Ibrahim Lipumba na Tundu Lissu,” alitamba Wasira.

Alisema hata katika mdahalo mwingine uliofanyika katika ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anaamini alifanya vizuri kuliko Lissu ambaye alikuwa akitetea msimamo wa upinzani waliokuwa wanataka muundo wa Serikali tatu.

Wasira alisema mchango wake mwingine ndani ya CCM ni kuongoza kamati ya wajumbe 20 wa chama hicho kuandika ilani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu 2015 ambayo ndiyo inatumika sasa.

“Nilikuwa mwenyekiti wa kutengeneza Ilani ya CCM, ambayo ndiyo inatumika sasa, hiyo ni ilani ya watu na nchi,” alisema Wasira.

Alisema kutokana na kukipigania chama hicho ndiyo maana wenzake wamekuwa wakimkubali na hata kumpigia kura nyingi katika nafasi ya ujumbe wa NEC.

Akizungumzia kushindwa kwake kutetea jimbo la Bunda na kuliacha likiangukia mikononi mwa Ester Bulaya wa Chadema, Wasira alilaumu alichokiita mchezo mchafu.

“Pesa nyingi ilitumika, wapinzani waliwanunua wasimamizi, mawakala, baadhi ya viongozi wa CCM na ndiyo maana wengine wamefukuzwa,” alisema Wasira.

“Kwa hiyo wanachama wenzangu wanataka kuonyesha dunia kuwa nilionewa na ndiyo maana wamenipa kura nyingi. Hii kazi haina malipo, ni shughuli ya kujitolea kwa ajili ya wanachama, lengo letu ni kujenga chama, na wakubwa wa chama hiki ni wanachama wenyewe,” alisema.

Wasira alisema jinsi watakavyoijenga CCM, itakuwa kazi ngumu kwa vyama vya upinzani kushinda katika chaguzi zijazo.

Wasira ameshika nafasi mbalimbali katika Serikali na chama ikiwa ni pamoja na kuwahi kuwa Waziri wa Kilimo.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger