Wednesday, December 20, 2017

Vyama vya Upinzani Vyamkosoa Mzee Makamba

Baadhi ya vyama vya upinzani vimekosoa kauli iliyotolewa juzi na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba vikisema imelenga kudhoofisha upinzani nchini.

Juzi, akihutubia Mkutano wa Mkuu wa CCM, Makamba alisema Rais mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa ‘anabatiza’ kwa maji, lakini Rais John Magufuli anafanya hivyo kwa moto na mfano mzuri ni uchaguzi wa marudio wa kata 43 ambao CCM ilizoa viti 42.

“Huu si ubatizo wa moto? Kazi tunayoifanya leo ni kuchagua kocha ambaye ni wewe (Rais Magufuli), kocha msaidizi Mangula (Philip) na Dk Shein (Ali Mohamed). Kama haitoshi unatakiwa uchague dawati la ufundi Kamati Kuu, sasa wenzangu wajue nimlisikia rafiki mmoja alikwenda kwa jimbo la Mnyika (John) na kusema 2020 njia nyeupe,” alisema mwanasiasa huyo.

“Njia nyeupe kwa utaratibu huu, kwa matokeo haya na ubatizo huu wa moto 2020 mshindi ni CCM we’ lala. Naomba mniruhusu niwaambie kina Mrema (Lyatonga), ubatizo ni uleule na leo sitaki kutabiri.Natabiri 2020 mheshimiwa Lowassa (Edward), Mbowe (Freeman) na Mapesa (John Cheyo ), John Shibuda wajue njia si nyepesi.”

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hakutarajia kama Makamba angetoa kauli hiyo kutokana na alichodai kuwa ni kuminywa kwa demokrasia nchini.

Alisema kinachofanyika sasa dhidi ya wapinzani ni sawa na refa anayechezesha mpira wa miguu kuwapa kadi nyekundu wachezaji wote wa timu husika, halafu timu nyingine inaendelea kucheza.

Naibu Katibu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema kauli hiyo haileti picha nzuri kwa siasa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema Makamba yupo sahihi na upinzani unabidi kufanya kazi ya ziada kama wanataka kushinda 2020.

“Tulikosea na tulichelewa kuunda upinzani, mwaka 1995 tulikuwa na nafasi nzuri sana ya kuungana kwa sababu hakukuwa na rais kama Magufuli, lakini sasa hivi yupo na sisi wapinzani tusipobadilika na siasa zetu za kususa watatuchapa kweli 2020,” alisema Mrema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo Bisimba alisema Makamba alisema ukweli kutokana na hali na mazingira ya siasa nchini.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger