Tuesday, December 19, 2017

Takwimu Zaonyesha Elimu Imesaidia Kupunguza Maambukizi ya VVU


 Elimu inayotolewa kwa wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na ugawaji wa nyenzo za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizopunguza maambukizi mapya kutoka asilimia 3.5 mwaka 2007 hadi kufikia 0.94 mwaka jana.

Mganga mkuu wa mgodi huo, Dk Mtemi Rusasa alisema hayo wakati wa upimaji VVU, saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti kwa wafanyakazi wa mgodi huo.

Rusasa alisema kila mwaka hufanya kampeni ya kupima afya na wafanyakazi 2500 hadi 3000 hujitokeza.


“Kwa takwimu hizi, kati ya wafanyakazi 100 mmoja anaweza kuwa na maambukizi au asiwapo, kwetu tunaona maambukizi yamepungua tofauti na mwaka 2007 ambayo ilikuwa kati ya 100 watatu walikuwa na maambukizi,” alisema Dk Rusasa.

Alifafanua kuwa mbali na huduma kwa wafanyakazi, GGM imekuwa ikisaidia jamii inayowazunguka kwa kutoa elimu ya VVU na kufanya matamasha ambayo wananchi hujitokeza kupima.

“Tumejenga VTC (vituo vya ushauri) mjini Geita, watu zaidi ya 300 hujitokeza kupima kwa mwezi na yule anayekutwa ameathirika huanzishiwa dawa, uelewa wa wananchi pia umekuwa mkubwa juu ya afya zao,” alisema Rusasa.

Baadhi ya wafanyakazi waliopima afya, Ester Maganga na Christian Michael walisema utaratibu ulioanzishwa na mgodi huo unawasaidia kujitambua kwa kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kupima afya.

Maganga alisema saratani ya kizazi imekuwa tishio nchini na kwamba ipo haja ya elimu kutolewa hadi vijijini ili wanawake wapimwe na kujua afya zao na wale wenye dalili wasaidiwe kupata matibabu kabla ya tatizo kuwa kubwa.

MWANANCHI
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger