Tuesday, December 19, 2017

"Sisi Tuliostaafu,Tukisikia Mivurugano Kwenye Chama Tunaweza Pata Magonjwa ya Moyo,” Kikwete


Dar es Salaam. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema hakuna shule ya urais na uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Amesema hayo  Jumatatu Desemba 18,2017 kwenye mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma.

Kikwete mbaye ni mwenyekiti mstaafu wa CCM akiwa wa kwanza kutoa salamu aliueleza mkutano huo kuwa hakuna anayesomea uenyekiti au urais ila mhusika anasoma akiwa ndani.

Amesema alitambua fika kuwa Rais John Magufuli ndiye mtu anayefaa kwenye nafasi hiyo licha ya kupata maswali kutoka kwa watu walioonyesha wasiwasi.

                                                                                   

Amesema, “Nilimtetea Magufuli watu walihoji hajawahi kuwa hata mjumbe wa shina iweje ghafla aje kuwa mwenyekiti wa chama. Nikawaambia ataweza kwani haiitaji shule.”

“Urais na uenyekiti hauna kwenda kusoma, unasomea humohumo ndani ukishapata ile dhamana, bora akili yako iwe nzuri ikiwa mbovu ndiyo inaweza kuleta shida, lakini huyu wa kwetu yupo vizuri tena kaongezea na PhD, tuna kila sababu ya kushukuru tumepata kiongozi mzuri,” amesema.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili, Magufuli amefanya mambo makubwa yanayoleta matumaini na ameonyesha ujasiri wa hali ya juu.

“Mpaka sasa ‘big up’ mtani wangu. Kazi hii ngumu sana, sababu mimi nimeifanya. Katika kazi ngumu duniani hii ndiyo kiboko. Uzuri na ubaya wa kazi hii ina upweke mkubwa,” amesema.

Kuhusu malalamiko ya hali ngumu ya maisha Kikwete amesema, “Kuweni na subira, viongozi wetu makini wanatambua matatizo yanayowakabili wananchi na ninaamini wanayatafutia ufumbuzi.”

Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM aligusia mwenendo wa chama hicho na kueleza kuwa wastaafu wanafarijika hali ya chama ikiwa shwari.

“Sisi tulistaafu faraja yetu kubwa ni kuona chama chetu kinaendelea kuwa imara. Tukija kwenye mikutano na watu wanafurahi na sisi mioyo inakuwa baridi. Lakini tukisikia mivurugano kwenye chama tunaweza pata magonjwa ya moyo,” amesema.

Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 facebook:

Post a Comment

Popular Posts

Copyright © MCHAMBUZI HURU | Powered by Blogger